Baraka FM

CHADEMA Mbeya yaituhumu CCM, Serikali kupanga kuvuruga uchaguzi

4 September 2024, 10:30

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya Masaga Pius Kamili(picha na Josea Sinkala)

Kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi Mkuu 2025 vyama mbalimbali vya siasa vimeendelea kujiandaa kuhakikisha vinashiriki chaguzi hizo.

Na Josea Sinkala, Mbeya

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya Masaga Pius Kaloli, amesema CHADEMA haitakubali viongozi wa kupita bila kupingwa katika chaguzi zijazo za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la mashauriano mkoa wa Mbeya alipoongoza kikao hicho cha kwanza tangu wachaguliwe.

Mwenyekiti huyo amesema kauli zinazoendelea kutolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri wa Habari Nape Nnauye kuwa matokeo yanategemea mtu anayehesabu na kutangaza kura pamoja na ile ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido kuwa madiwani wa Wilaya hiyo walipita bila kupingwa mwaka 2020 ni Mungu anaendelea kuwaumbua.

Pamoja na mengi aliyoyaongea amewataka wana-Chadema na wananchi kwa ujumla kuendelea kujiandaa na chaguzi hizo hasa uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kuhakikisha wakati utakapowadia wajiandikishe na kujitokeza kuchagua viongozi bora na kulinda kura.

Katika kikao hicho wamezindua mpango kabambe wa K3 unaolenga kuhimiza wananchi Kujiandikisha na kulinda kura wakati ukifika.

Naye mwenyekiti wa Baraza la wazee wa CHADEMA (BAZECHA) mkoa wa Mbeya John David Mwambigija amewataka wazee wote katika mkoa huo, viongozi wa Chama na mabaraza na wanachama kwa ujumla kuendelea kushikamana ili kuhakikisha CHADEMA inashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la vijana (BAVICHA) mkoa wa Mbeya Evaristo Elisha Chonya amewataka vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kwenda kuwa sehemu ya maamuzi na kuwa na hatma bora ya Taifa lao kuanzia Serikali za mitaa hadi uchaguzi mkuu na kusisitiza kulinda kura kipindi cha chaguzi.

Hiki ni kikao cha kwanza cha Baraza la mashauriano mkoa wa Mbeya tangu kuchaguliwa kwa uongozi mpya wa CHADEMA mkoa wa Mbeya ambapo baraza hili la uongozi linakabiliwa na masuala ya uchaguzi wa Serikali za mitaa vitongoji na vijiji baadaye Novemba mwaka huu ikiwa ni majirio ya uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 pamoja na mikakati mbalimbali ya kuendelea kukijenga chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania hasa upande wa bara.