Baraka FM

Diwani kata ya ilima Tukuyu azikwa,madiwani wenzake wamlilia

1 September 2024, 11:19

Mwili wa marehemu Philipo Shimwela ukipelekwa eneo la kaburi tayari kwa kuzikwa

Kifo ni fumbo ambalo hakuna anayeweza kutegua fumbo hilo isipo kuwa Mungu mwenyewe anayetoa na kutwaa.

Na Hobokela Lwinga

Aliyekuwa Diwani wa kata ya Ilima Marehemu Philipo Shimwela amezikwa tarehe 31.8.2024 katika kijiji chao cha Lubanda kilichopo katika kata hii Barabara ya Tukuyu-Kyela.

Marehemu Shimwela amehudumu katika kata hii tangu mwaka 2020 na katika kipindi hiki amesaidia upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Kayuki , Ilima sekondari na Msingi barabara ya Tukuyu-Kyela.

Ukarabati na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Kinyangwa kupitia Mradi wa COCOA FOR SCHOOL.

Pamoja na hayo aliendelea kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji kupitia visima vifupi na virefu pamoja na mradi wa maji mserereko kupitia mradi wa Masoko Group.

Aidha vijiji vyote katika kata ya Ilima vinapata huduma ya Umeme na kila kijiji kina zahanati yake hatua inayosaidia kupata huduma matibabu karibu na makazi yao.

Marehemu Shimwela katika enzi ya uhai wake pia aliendelea na zoezi la kuhakikisha kila kaya inapanda miche ya Mikorosho, na Kakao ili kujikwamua kiuchumi.