Wananchi Tukuyu kunufaika na mradi wa maji
28 August 2024, 15:19
Maji Ni Uhai Kila Mtu Anapaswa Kulinda Na Kutunza Vyanzo Vya Maji Ikiwa Ni Sambamba Na Kulinda Miradi Ambayo Iko Kwenye Maeneo Yao.
Na Hobokela Lwinga
Mwenge wa uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika mji wa Tukuyu unaosimamiwa na mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Mbeya.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Eliakimu Mnzava amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kusogeza karibu huduma ya majisafi kwa wananchi hivyo miradi lazima ikamilike.
Naye Benard Konga Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBEYAUWSA) amemshukuru Rais Dr.Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo na kwamba hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM.
Aidha Mbunge wa Rungwe Anthony Mwatona ameiomba serikali kuongeza nguvu kwenye mradi huo ili ukamilike kwa wakati na wananchi wapate manufaa ya maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya CPA Gilbet Kayange amesema mamlaka ya maji Tukuyu ilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni tano hivyo utekelezaji wa mradi huo utaweza kuzalisha lita milioni nane.