Taarifa za kushushwa hadhi mamlaka ya mji mdogo Kyela zazua taharuki
20 August 2024, 19:12
Mamlaka ya mji mdogo wa Kyela ni miongoni mwa miji inayopatikana mkoani Mbeya ambapo badala ya kupanda hadhi ili kuwa halmashauri mji huo unashushwa katika nafasi hiyo.
Na Hobokela Lwinga
Wananchi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Kyela mkoani Mbeya wameiomba serikali kuiacha mamlaka ya mji huo kuendelea kuwahudumia kwa ukaribu kutokana na uwepo wa taarifa za kutaka kuifuta mamlaka hiyo.
Wamesema uwepo wa mamlaka hiyo umesaidia kuinua uchumi na maendeleo katika eneo lao hivyo wamesikitishwa na taarifa za kutaka kuifuta.
Aidha wamemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo kwa kuwa lina umuhimu mkubwa kwao.
Emmanuel Bongo ni mwenyekiti wa mamlaka hiyo anasema hii siyo mara ya kwanza kuibuka kwa taharuki kama hii ya kutaka kufutwa kwa mamlaka yao kutokana na vikao vya maamuzi vya baraza la madiwani na kupitisha nyaraka ambazo wao kama mamlaka ya mji mdogo hawajazipitisha.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya Kyela Ndugu Katule Kingamkono amesema wananchi wanapaswa kuwa watulivu wakati suala hilo linafanyiwa kazi.