Mbunge Sichalwe awawezesha vijana kiuchumi
23 July 2024, 13:12
Kongamano la kuwawezesha vijana kiuchumi lavunja rekodi kutokana na idadi kubwa ya vijana waliojitokeza.
Na mwandishi wetu, Momba Songwe
Mamia ya vijana kutoka makundi na kanda mbalimbali wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Momba Mheshimiwa Condester Sichalwe (Mundy) kwa kuandaa kongamano maalumu la kuwawezesha kiuchumi Vijana wa Halmashauri hiyo.
Miongoni mwa makundi ya vijana waliopata fursa ya kufikiwa na mafunzo ya uwezeshwaji kiuchumi ni, Walimu wakuu na wakuu wa shule zote za msingi na Sekondari za Halmashauri ya Momba, Watendaji wa Kata zote 14 na Vijiji 72, Madereva Bodaboda, Vyama vya Ushirika na Jumuiya za vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Momba.
Mbunge Sichalwe amesema katika kongamano hilo aliwaalika wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, kama vile, taasisi za kifedha, yaani NMB, CRDB, SELF MICROFINANCE, pia taasisi zingine kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIR), Wakala wa Usalama Afya mahala pakazi (OSHA), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Jeshi la Polis, TAKUKURU na Chama cha Ushirika mkoa wa Songwe.
Sichalwe amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa na kuonyesha fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana wa Jimbo la Momba, ili waweze kuzifahamu na kuzichangamkia kwa ajili ya kuongeza vipato vyao na kuendelea kukuza uchumi wa jimbo hilo.
“Mimi ni Mbunge kijana ambaye nimebahatika kuzunguka nchi nyingi duniani, wakati napita huko nimekutana na fursa mbalimbali za kiuchumi kama hii tulioifanya leo, hivyo niliona nisiwe mchoyo wa kugawa fursa hizi kwa watu wangu wa Momba, ndiyo maana nimeona ni vema kuwa na kongamano hili la kuwafungulia milango vijana wenzangu, tumeamua kutumia gharama kubwa kufanikisha jambo hili kwa maslahi mapana na watu wangu ninao waongoza “Sichalwe.
Baadhi ya vijana wamemshukuru Mbunge kwa kuja na fursa kwa madai kuwa huenda amevunja rekodi kwa kuwa Mbunge wa kwanza kwa Jimbo la Momba kuja na wazo hilo, na kueleza kuwa wataendelea kumuunga ili kufanikisha azma yake ya kuipeleka mbele Halmashauri ya Momba kimaendeleo.