Baraka FM

Wakulima, wafanyabiashara watakiwa kuongeza umakini katika biashara zao

26 June 2024, 12:54

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP ) Anthony Mkwawa (kushoto)na kulia ni Mkaguzi wa Polisi Frida Mng’anya wakiwa katika studio za radio Baraka Fm(picha na Hobokela Lwinga)

Duniani kote binadamu amekuwa akifanya jambo ili kupata tija ya kile anachokifanya ndivyo ilivyo katika uzalishaji wa mali kupitia kilimo ambapo wapo wakulima wamekuwa wakilima mazao kwa ajili ya biashara aua chakula.

Na Hobokela Lwinga

Wakulima na wafanyabiashara wa mazao mkoani Mbeya wametakiwa kuwa makini katika shughuli zao za biashara ili kuepuka uhalifu.

Akizungumza Juni 25, 2024 kupitia Kituo cha Redio Baraka FM Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP ) Anthony Mkwawa akiwa na Mkaguzi wa Polisi Frida Mng’anyi wamesisitiza na kuwataka wakulima na wafanyabiashara wa mazao mbalimbali kuongeza umakini katika shughuli zao za biashara hasa katika kipindi hiki cha mavuno.

Kamishina Msaidizi wa Polisi Mkwawa ameelezea kuwa katika kipindi cha msimu wa mavuno mara nyingi hutokea matukio ya kihalifu ikiwemo unyang’anyi, uporaji wa fedha kwa wanunuzi wa mazao pamoja na wizi hivyo ni vyema kuchukua tahadhari na kuongeza umakini.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP ) Anthony Mkwawa(Picha na Hobokela Lwinga)

Vile vile, Kamishina Msaidizi wa Polisi Mkwawa amewataka wananchi na wafanyabiashara Mkoani humo kuwa na desturi ya kuhifadhi fedha zao katika Benki mbalimbali ambapo kimsingi ndio salama zaidi kuliko kuhifadhi majumbani au kutembea na fedha nyingi kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Naye, Mkaguzi wa Polisi Frida Mng’anya ameelezea kuwa katika kuhakikisha wakulima na wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu amewataka wananchi hao kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili zifanyiwe kazi.

Sambamba na hilo amesisitiza na kuwataka wananchi kufanya shughuli ambazo zitawaingizia kipato halali kuliko kujihusisha na vitendo vya kihalifu ambavyo kamwe havitawafikisha popote zaidi ya kukutana na mkono wa sheria na kufungwa.