DC Songwe akemea wanaoendekeza ushirikina
25 June 2024, 06:59
Kutokana na changamoto za mmonyoko wa maadili ulimwenguni wakristo wameombwa kuendelea kuombea watu wanaojihusisha na vitendo vya kishirikina ikiwemo ubakaji watoto na ushoga.
Na Ezra Mwilwa
Mkuu wa wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mheshimiwa, Daniel Chongolo katika Mkutano Mkuu wa injili, uliyofanyika katika shule ya msingi Ichenjezya mji wa Vwawa Mkoani Songwe huku akikemea baadhi ya watu wenye imani potofu wanaofanya vitendo vya ubakaji katika jamii.
Mkutano huo ambao umefanyika leo Jumapili Juni 23, 2024 umeandaliwa na New Life in Christ, Muungano wa makanisa mbalimbali ya kikristo nchini.
Katika mkutano huo, Mhe. Itunda amewapongeza viongozi na wananchi walioshiriki mkutano huo kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano huku akikemea baadhi ya watu wenye imani potofu wanaofanya vitendo vya ubakaji na ulawiti katika jamii wakiamini kuwa watapata fedha.
Akiwasilisha salamu za Rais wa JMT, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, DC Itunda ameeleza kuwa Rais Samia anatambua kazi inayofanywa na viongozi wa dini ndiyo maana amekuwa akishirikiana nao katika mambo mbalimbali.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Mbozi Mhe Esther Mahawe na Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Konde Askofu Geofrey Mwakihaba.