Baraka FM

Ken Gold FC kukamilishiwa ujenzi uwanja na halmashauri ya wilaya ya Chunya

24 June 2024, 18:12

Mwonekano wa uwanja unao tarajiwa kujengwa Chunya(picha na Ezekiel Kamanga)

Chunya imepania kukamilisha zoezi la ujenzi wa uwanja kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu Tanzania, yatenga Tsh.200 milioni.

Na Ezekiel Kamanga
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Tamim Kambona amesema Halmashauri yake imetenga shilingi milioni mia mbili kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa michezo uliopo kata ya Mbugani unaomilikiwa na Halmashauri ili ukamilike kabla ya kuanza kwa ligi kuu mwaka 2024/2025 utakaotumiwa na timu ya Ken Gold iliyopanda daraja msimu huu.

Akizungumza na kituo hiki Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya amesema mbali ya kutenga fedha hiyo kupitia mapato yake ya ndani pia imeunda kamati ya wadau inayoongozwa na Ayoub Omary.

Kambona amesema sanjari na mipango ya kamati Halmashauri inatarajia kutenga fedha nyingi zaidi mwaka ujao wa fedha ambapo uwanja huo wa kisasa utatandikwa zuria kwa ajili ya mpira wa miguu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mkoani Tamim Kambona(picha na Ezekiel Kamanga)

Aidha amewashukuru wadau wadau ambao wanatoa michango ya hali na akiwemo mwekezaji wa madini David Mathayo ambaye ametoa tingatinga kwa ajili ya kushindilia uwanja.

Kambona amewataka wananchi kuungana ili kuhakikisha uwanja unakamilika kabla ya mashindano ambapo wananchi wataongeza mapato yao kutokana na ujio wa wageni kutoka nje ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla.

Boniphace Mwinuka mkazi wa Kata ya Chokaa na mfanyabiashara amesema kitendo cha kupanda daraja kwa timu ya Ken Gold kuleta hamasa kubwa ya michezo katika Wilaya ya Chunya kwani wengi wao walikuwa wakisafiri kwenda Mbeya ili kuona michezo ya ligi kuu.

Amesema wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni watapokea wageni wengi pia wajasiriamali na madereva wa Bodaboda nao watasafirisha abiria kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chunya.

Eneo linalo tarajiwa kujengwa uwanja Chunya utakao tumiwa na Timu ya Ken Gold(picha na Ezekiel Kamanga)

Timu ya Ken Gold inayonilikiwa na Keneth Mwakyusa iliongoza ligi ya NBC na kufanikiwa kupanda daraja na hii ni timu ya kwanza kucheza ligi kuu kutokea Wilaya ya Chunya.

Mkoa wa Mbeya umebakiwa na timu mbili baada ya timu ya Ihefu kuuzwa na kuhamisha mavazi yake mkoani Mbeya