Kampuni ya ununuzi pareto yatoa mafunzo kuelekea msimu mpya wa ununuzi
10 June 2024, 12:25
Kampuni ya ununuzi wa zao la pareto Tanzania PCT imefanya kikao kazi na mawakala wake kuelekea msimu mpya wa uvunaji ambao unaanza july mosi 2024 ili kuweza kupata maua bora ya zao hilo.
Kikao kazi hicho kilichoandaliwa na kampuni ya ununuzi wa zao la Pareto PCT kimefanyika katika ukumbi wa IADO kijiji cha santilya halmashauri ya wilaya ya Mbeya.
Gerald Joseph ni mhasibu mkuu wa PCT ametumia fursa ya kikao hicho kuwaomba mawakala wa kampuni yake kufuata sheria za ununuzi wa pareto yenye ubora huku afisa Pareto wa Songwe na Mbeya Musa Malubalo akiwataka wakulima kuepuka kuchuma maua ambayo hayajakomaa huku akisema kampuni yake imejipanga kutoa vikaushio 200 vitavyosaidia ukaushaji bora wa zao hilo.
Miongoni mwa wakulima walioshiriki kikao kazi hicho wamehoji kwanini makampuni mengine hayatoi mafunzo kwa wakulima?swali hilo limejibiwa na bwana shamba kutoka bodi ya pareto Tanzania Edwin Mangwe kwamba kila mnunuzi anapaswa kuweka alama ya utambuzi wa kituo cha ununuzi.
Baadhi ya mawakala Wameiomba serikali kuyasimamia makampuni ya ununuzi ili yaache kununua Pareto isiyo na ubora na wazingatie kanunuzi na sheria za ununuzi wa zao hilo.
Kutokana na baadhi ya wakulima kuchuma maua yasiyokomaa na kuuza Pareto mbichi kwa mwaka 2023 kampuni ya PCT ilistisha zoezi la ununuzi katika halmashauri ya wilaya ya Mbeya na kwasasa inatarajia kuanza zoezi la ununuzi July mosi 2024.