Mzazi atakaye ozesha mwanafunzi kufungwa jela miaka 30 Mbeya Dc
30 May 2024, 18:47
Wahenga wanasema elimu ni msingi wa maisha wengine wanasema elimu ni ukombozi, Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza kiwango cha ufaulu ambacho kitatokomeza ziro.
Na Hobokela Lwinga
Kata ya shizuvi halmashauri ya wilaya ya Mbeya imezindua mpango kazi wa elimu wa miaka mitatu idara ya elimu ya msingi ngazi ya kata 2024-2026 lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha ufaulu katani hapo.
Akizungumza akiwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo afisa elimu wilaya ya Mbeya Tanu Kameka amewataka wazazi kuwa na kipaumbele cha elimu kwa watoto wao badala ya kuwaozesha wakiwa bado hawajatimiza ndoto zao za elimu.
Aidha mwalimu Kameka amewataka wanafunzi kuacha kubweteka badala yake wazingatie elimu kwa kusoma kwa bidii.
Awali akisoma taarifa ya kata kwa mgeni rasmi, afisa elimu kata ya shizuvi Mwalimu Joel Gabriel Munuo amesema kutoka na kata hiyo kutilia umakini suala la elimu limesababisha utoro kwa wanafunzi kupungua.
Kwa upande wake diwani wa kata ya shizuvi mhe.Noah Mwashibanda amesema kupanda kwa elimu katika kata yake kumesababishwa na wananchi kutoa ushirikiano kwa viongozi ikiwa ni sambamba na mwitikio wa kutoa chakula cha wanafunzi kula shuleni.
Katika uzinduzi huo mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza 2023 Anyangison Adaison Mlili amepewa motisha ya shilingi laki moja kutoka kwa mbunge alan njeza na fedha zingine kutoka kwa wadau waliojitokeza kwenye hafla hiyo.