TADIO yawaasa wanahabari kutumia kalamu zao kwa weledi
25 April 2024, 20:41
Kufuatia ukuaji wa sayansi na teknolojia duniani, tasnia ya habari ni moja ya tasnia inayotakiwa kwenda sambamba na mabadiliko hayo katika kuzingatia taaluma yao kuwa karibu na jamii wanayoitumikia kwa kuwalisha habari zenye ukweli na uhakika.
Na Hobokela Lwinga
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kwa weledi na kufuata maadili ya taaluma yao kutokana na taaluma hiyo kuaminiwa kwa kiasi kikubwa na jamii.
Wito huo umetolewa na mkufunzi Hilali Ruhundwa kutoka mtandao wa redio jamii wa TADIO wakati akitoa mafunzo kwa watangazaji na waandishi wa habari wa kituo cha redio Baraka FM kilichopo Kadege jijini Mbeya.
Ruhundwa amesema misingi ya taaluma ya uandishi wa habari ni kuandika kitu chenye ukweli na uwazi.
Aidha Ruhundwa amesisitiza kuwa kuelekea kipindi cha uchaguzi waandishi wa habari wazingatie usawa wa kutoa habari kwa vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wafanyakazi, meneja wa redio Baraka FM Charles Amulike amewataka washiriki kuzingatia mafunzo waliyoyapata.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo kwao yameongeza chachu ya utendaji katika kutekeleza majukumu yao ya kuuhabarisha umma.