Zaidi ya ekari 100 za mazao zaharibiwa na mdudu hatari Mbozi
19 April 2024, 17:54
Mdudu anayefanana na funza anakula mizizi ya mazao yote ya Chakula ,Biashara na mbogamboga ambapo wakulima wameingiwa na hofu ya kuendelea kulima kutokana na uwepo na mdudu huyo hatari Kwao.
Na Mwandishi wetu Songwe
Zaidi ya ekari 100 za mashamba ya wakulima ya mazao ya Chakula na biashara katika kijiji cha ikomela kata ya kilimampimbi Wilayani Mbozi Mkoani Songwe yameharibiwa na mdudu aina ya funza ambaye amekuwa akiharibu mizizi ya mazao na kufanya mazao hayo kudondoka chini na mengine kunyauka na kushindwa kuzalisha hali ambayo imetajwa kuwarudisha nyuma wakulima hao na kuwakatisha tamaa ya kuendelea kulima.
Wakulima hao wamepaza sauti zao kwa serikali na kuomba kupatiwa suluhu ya mdudu huyo ambaye anadaiwa kuwepo kwa takribani miaka kadhaa sasa hali ambayo imesababisha wakulima hao kukata tamaa ya kuendelea kulima kutokana na uwepo na mdudu huyo mharibifu wa mazao ya wakulima huku wakipata hasara kutokana na gharama wanazotumia katika Kilimo .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho cha ikomela Bwana Watson Sichone amesema kama serikali ya kijiji tayari imechukua hatua dhidi ya changamoto hiyo ikiwemo ya kutoa taarifa katika idara ya kilimo huku akikiri kuwa mashamba mengi yameharibiwa na mdudu huyo.
Akitolea ufafanuzi wa mdudu huyo na namna idara ya Kilimo wilaya ilivyochukua hatua dhidi ya mdudu huyo Afisa Kilimo Wilaya ya Mbozi Tito Njowela amesema wamepokea taarifa hizo na tayari zimeshafikishwa kwenye Mamlaka zinazohusika huku akitoa ufafanuzi wa namna ya kuchukua hata za awali ili kudhibiti mdudu huyo.