Polisi Mbeya wapokea vitendea kazi kutoka Lulu saccos
14 March 2024, 14:24
Kila mwananchi anapaswa kushiriki shughuli za ulinzi kwa namna yoyote ile,ikiwa huwezi kushiriki kwa nguvu basi unapaswa kujitoa kwa mali hivi ndivyo taasisi ya fedha ya lulu saccos imeamua kushiriki kuimarisha ulinzi kwa kulipatia jeshi la polisi vitendea kazi.
Na mwandishi wetu
Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Lulu Saccos cha Jijini Mbeya kimetoa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya chama hicho.
Akizungumza Machi 13, 2024 wakati wa kukabidhi vitendea kazi hivyo ambavyo ni taa 20 za kuongozea magari wakati wa usiku na karatasi (Rim Paper) katoni tano, Mwenyekiti wa Lulu Saccos ndugu Oberd Mtweve amesema kuwa ni utaratibu wa chama hicho kurejesha kwa jamii kila mwaka.
Aliongeza kuwa, mwaka huu wameguswa na kuona umuhimu wa kulifikia Jeshi la Polisi hasa upande wa Kikosi cha usalama barabarani na kuwiwa kutoa vitendea kazi, taa 20 za kuongozea magari wakati wa usiku.
“Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa, kama Lulu Saccos tumeona umuhimu wa kutoa kidogo kilichopatikana kutoka kwa wanachama zaidi ya 2,000 wa chama hiki cha ushirika, Askari hasa wakati wa usiku wamekuwa wakiongoza magari bila kutumia taa maalum hivyo tumeona umuhimu wa kutoa vifaa hivi ” alisema Mtweve.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga ameshukuru kwa msaada wa vifaa hivyo na kuahidi kwenda kuvitumia vizuri ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Mbali na Jeshi la Polisi, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Shule ya Sekondari Samora na Kituo cha kulelea watoto yatima cha Nuru Orphans Centre cha Jijini Mbeya walikabidhi vifaa na mahitaji mbalimbali kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Lulu Saccos.