Baraka FM

Rungwe yazindua chanjo ya minyoo, kichocho

29 February 2024, 17:06

Na mwandishi wetu

Mkuu wa wilaya ya Rungwe Mhe. Jaffar Haniu tarehe 28.2.2024 amezindua zoezi la chanjo ya minyoo na kichocho ikiwa ni sehemu ya kutokomeza magonjwa yote yasiyopewa kipaumbele katika jamii.

Zoezi hili limefanyika katika shule ya msingi Katumba Mchanganyiko kata ya Ibighi.

Akizindua zoezi hili Mhe. Haniu ameagiza wazazi wote kuwapeleka watoto katika maeneo ya kutolea huduma hii ikiwemo hospitali, zahanati na vituo vya afya sambamba na shule zote za msingi na sekondari.

Amesema kila mzazi hana budi kuhakikisha mtoto anapata chanjo hii zikiwa ni jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata afya bora na stahiki kwa wakati.

Mhe Haniu amewakumbusha wazazi pamoja na walimu wakuu kuhakikisha watoto wanakula chakula cha kutosha kabla ya kupewa chanjo hii.

Hata hivyo amewaondoa shaka wazazi wote kuwa chanjo hii na zingine zinazotolewa na serikali hazina madhara yeyote kwa watoto badala yake huimarisha afya yao na maisha bora zaidi kwa miaka mingi mfululizo.Chanjo hii ambayo itatolewa kwa muda wa siku mbili itajumuisha watoto kuanzia miaka 05 mpaka miaka 14.