Chunya yaongoza ukusanyaji mapato mkoa wa Mbeya
29 February 2024, 16:43
Na Mwandishi wetu
Halmashauri ya wilaya ya Chunya imeendelea kuziongoza halmashauri za mkoa wa Mbeya katika ukusanyaji wa mapato kwa tofauti ya zaidi ya asilimia arobaini (40%) baada ya kukusanya shilingi bilioni 7.3 sawa na asilimia 133 kwa kipindi cha kuanzia Julai mosi mpaka tarehe 23 Februari 2024 huku halmashauri ambayo inafuatia ikiwa na asilimia 90 ya makusanyo.
Kwa mujibu wa takwimu zinazotolewa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya juu ya mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri za Mkoa wa Mbeya kuanzia julai mosi 2023 mpaka februali 23 Halmashauri ya wilaya ya Chunya kwa kipindi chote cha mwaka huu imeendelea kuongoza na kwa sasa inaongoza kwa tofauti ya asilimia arobaini (40%).
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya amekuwa kinara wa kuhimiza watumishi anaowaongoza kufanya kazi kwa weledi, kujituma na kwa uzalendo huku akiwataka kuheshimiana, kuheshimu kanuni na taratibu za utumishi wa umma jambo ambalo limekuwa chachu kubwa ya mafanikio ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya katika Nyanja mbalimbali ikiwepo ukusanyaji wa Mapato
Halmashauri ya wilaya ya Chunya itaendelea kuongoza Mkoa wa Mbeya katika ukusanyaji wa Mapato hata mwaka ujao yaani 2024/2025 kutoka hali ya zao la Tumbaku kuwa ya Kuvutia na kuridhisha Mashambani jambo linalotoa taswira ya Mafanikio makubwa ya mavuno ukilinganisha na mwaka jana yaani 2023/2024 ambapo Halmashauri ya wilaya ilikusanya Zaidi ya shilingi bilioni mbili kutokana na kilimo cha Tumbaku
Aidha kutokana na makusanyo yanayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato Halmashauri ya wilaya imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali kupitia mapato yake ya Ndani, miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Shule ya Mchepuo wa Kiingeleza, Ujenzi wa Kituo cha afya sangambi na miradi mingine hivyo kuendelea kuimarika katika ukusanyaji wa mapato ni ishara tosha ya mwendelezo wa ujenzi wa miradi zaidi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya ili kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazo wakabili wananchi katika maeneo yao.