Baraka FM

CPA. Cecilia Kavishe amefanya kikao na timu ya menejimenti ya Shule ya Sekondari ya Maweni

22 February 2024, 14:59

Na mwandishi wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, CPA. Cecilia Kavishe amefanya kikao na timu ya menejimenti ya Shule ya Sekondari ya Maweni kujadili namna bora ya kuendesha shule hiyo, kuimarisha mahusiano na kusikiliza changamoto za shule hiyo.Kikao hicho kimefanyika leo Alhamisi Februari 22, 2024 katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.

Akizungumza baada ya kikao hicho, CPA Kavishe amesema “Leo nimekutana na timu ya menejimenti ya Shule ya Sekondari Maweni nikiwasilikiliza na kujadili namna ya uendeshaji wa shule ambayo ni mojawapo ya shule yenye wanafunzi wengi kuanzia kidato cha kwanza hadi sita.

Dhumuni ni kuweka mahusiano mazuri kati ya uongozi wa shule hiyo na kuweka malengo mazuri yatakayopelekea ufaulu mzuri.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Namnyaki Laitetei, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Chance Kiula pamoja na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Shemgei Sheghagilo.CPA.

Kavishe ameisisitiza umoja, uwazi na upendo katika kusimamia taasisi na kuiagiza menejimenti kusimamia malezi bora ya wanafunzi ambao taifa linahitaji waje kuwa wataalamu na viongozi bora wa baadae katika kada mbalimbali wakilitumikia taifa kwa uzalendo na uadilifu.

Mkurugenzi huyo amekuwa na utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na watumishi na kuzifanyia kazi, ambapo kila Jumanne akiambatana na wataalamu anafanya kata kwa kata kusikiliza kero na kila Jumatano anasikiliza kero za mmoja mmoja akiwa ofisinI.