Yanga yaadhimisha miaka 89, yatoa msaada hospitali ya kanda Mbeya
10 February 2024, 16:53
Na Hobokela Lwinga
Kuelekea maadhimisho ya miaka 89 tangu kuanzishwa kwa klabu ya mpira wa miguu ya Yanga, leo 10 Februari, 2024 wanachama pamoja na viongozi wa kitaifa wa klabu hiyo wametembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Kitengo cha Huduma ya Mama na Mtoto Meta kwa lengo la kufanya usafi pamoja na kutoa zawadi kwa wagonjwa waliolazwa katika kitengo cha watoto wachanga Meta.
Akiongea baada ya zoezi hilo Ali Kamwe, Msemaji wa klabu ya mpira wa Yanga ameushuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa kuonyesha ushirikiano mzuri katika kufanikisha tukio hilo na kuwaasa wanachama wa klabu hiyo kujenga tabia ya kurudisha kwa jamii kile kinachopatikana kwa kuwa kufanya hivyo ni ibada.
“..Tuhamasishe kwenye matawi yetu kufanya ibada za namna hii, tutembelee watu wenye mahitaji na hiyo itakuwa na malipo mazuri siku ya mwisho.” – Ali Kamwe
Nae Dkt. Uwesu Mchepange, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali, ameushukuru uongozi wa klabu ya Yanga pamoja na wananchi wote walioshiriki kwa pamoja katika zoezi hili la kufanya usafi na kutoa zawadi kwa wagonjwa kwa kuchagua hospitali hiyo kati ya hospitali nyingi zinazopatikana mkoani Mbeya.
“..Hapa Mbeya kuna hospitali nyingi sana, lakini kati ya Hospitali hizo nyingi mmechagua kuitembelea hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa hiyo sisi tunajihisi wenye bahati sana.” – Dkt. Uwesu Mchepange
Dkt. Erica Balama ni Daktari Bingwa wa Watoto Wachanga kitengo cha Huduma ya Mama na Mtoto Meta, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uboreshaji wa miundo mbinu mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na hivyo wananchi kuendelea kupata huduma bora pamoja na kuwashukuru wanachama pamoja na viongozi wa klabu ya Yanga kwa zoezi hilo la kufanya usafi pamoja na kutoa zawadi kwa wagonjwa katika kitengo hicho cha watoto wachanga.
“..Tungependa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa uboreshaji mkubwa wa miundombinu pamoja upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuushukuru uongozi wa Yanga kwa zoezi hili.”