Matukio 53 ya ajali yaripotiwa kutokea mwaka 2023 Mbeya
18 January 2024, 11:23
Na Ezekiel Kamanga
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya SF Malumbo Ngata ametoa taarifa ya miezi sita ya matukio mbalimbali hamsini na tatu yalliyoripotiwa Mkoani Mbeya likiwemo la vifo vya watoto wawili waliofariki baada kutumbukia kisima cha maji.
Ngata amesema kati ya matukio hayo arobaini na sita ni ya ajali za moto ambazo nyingi zimetokana na uzembe hususani watoto kuchezea mishumaa na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Aidha Kamanda Ngata amesema baadhi ya mabweni yalichomwa kwa makusudi kutokana na ukosefu wa maadili kwa baadhi ya wanafunzi.
Hata hivyo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya limeendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali kama shule za msingi,sekondari ,vyuo,masoko,vituo vya mabasi na maeneo ya maegesho ya maroli.
Ngata amewataka wananchi kuitumia vizuri namba ya dharula 114 badala ya kuitumia namba hiyo kufanya dhihaka hivyo walati wengine wakihitaji huduma wao hiitumia vibaya.
Kamanda Ngata amesema Jeshi la Zimamoto limeendelea kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Mbeya hususani maeneo ya machimbo kama Chunya sanjari na maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko kama Kyela na Mbarali.
Katika hatua nyingine Ngata amesema ujenzi holela umekuwa kikwazo kwa Jeshi la Zimamoto kushindwa kuyafikia maeneo pindi zinapotokea ajali.
Malumbo amesema kwa kushirikiana na mipango miji wamekuwa wakishauriana ili kuhakikisha miundo mbinu ya barabara inakuwa rahisi kufikika.
Ngata amesema wamefanya ukaguzi katika shule mbalimbali kuhakikisha mabweni yana vizimia moto pia kuzuia matumizi ya simu kwa wanafunzi ili kuzuia ajali.
Kamanda Malumbo Ngata amewataka wananchi kuacha kupambana na majanga wao wenyewe badala yake watoe taarifa mapema kupitia namba ya dharula 114 ili waweze kufika mapema eneo la tukio.
Nao baadhi ya wananchi Jijini Mbeya mbali ya kulipongeza Jeshi la Zimamoto kwa utendaji mzuri wameiomba serikali kuliboreshea vitendea kazi ili Jeshi liwe la kisasa zaidi kukabiliana na majanga.
Festo Mwakyusa mkazi wa Iyela ameiomba serikali kuboresha mifumo ya maji hasa maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kama shule,masoko na kumbi za starehe.
Amesema elimu inayotolewa na Jeshi la Zimamoto imesaidia kuelewa matumizi sahihi ya majiko ya gesi na matumizi ya vizimia moto.
Naye Tabitha Bugali mkazi wa Forest amesema hivi sasa wanafunzi wanajengewa uwezo ambapo sasa wanaelewa namna ya kukabuliana na majanga.Bugali amewataka wazazi kuwa waangalifu hasa mashimo ya visima hasa kipindi hiki cha mvua.