Wanafunzi 11 wa darasa la 7 wanusurika kifo baada ya kupigwa na radi Iringa
16 January 2024, 09:53
Na Moses Mbwambo, Iringa
Watoto 11 ambao ni wanafunzi wa darasa la 7 katika Shule ya Msingi Uyole kata ya Kitwilu iliyopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wamenusurika kifo baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani wakati mvua ikinyesha katika eneo hilo.
Katika tukio hilo mwalimu naye ambaye alikuwa na watoto hao darasani alijeruhiwa.
Halima Omari Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Iringa akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU) amefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ambapo watoto hao wamefikishwa kwa ajili ya matibabu amewata wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakati huu mvua zikiendelea kunyesha.
Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Huruma Mwasipu amesema watoto hao wamepatwa na majeraha ya kuungua maeneo mbalimbali ikiwemo mikononi.