Kamati ya uongozi ya REGROW yaridhishwa na maendeleo ya mradi Mikumi
21 December 2023, 08:16
Na mwandishi wetu
Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) imetembelea na kujionea utekelezaji wa Mradi huo, katika Hifadhi ya Taifa Mikumi na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema licha ya kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kiwanja cha ndege Hifadhini hapo kamati hiyo imemtaka mkandarasi kuhakikisha uwanja huo pamoja na miundombinu mingine unamalizika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa na kutambua kuwa hakuna muda wa ziada utakao ongezwa kwa ujenzi wa uwanja huo.
Dkt. Abbasi amesisitiza kuwa kukamilika kwa wakati kwa uwanja huo ni hatua muhimu ya kutimiza lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwaletea maendeleo zaidi watanzania kupitia sekta ya utalii na kuimarisha uhifadhi wa Maliasili nchini.
Akizungumzia uwezo wa uwanja huo wenye urefu wa Kilomita 1.8, Dkt. Abbasi amesema utakapokamilika, utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege tisa, kupokea abiria 160 kwa wakati mmoja, hali itakayopelekea watalii wengi kumiminika kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi na vivutio vya jirani.
Aidha Dkt. Abbasi ameongeza kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya The Royal Tour, inaenda sambamba na maandalizi ya kupokea watalii wengi zaidi kwa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania kupitia mradi wa REGROW.
Naye Mhandisi Peter Mrosso wa kampuni ya Badr East African Enterprises Ltd inayojenga uwanja wa ndege Hifadhi ya Taifa Mikumi, ameipongeza kamati hiyo kwa kutembelea mradi, na kuwa Ofisi yake itayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na kuhakikisha inakabidhi uwanja na miundombinu mingine kwa wakati uliopangwa.
Kamati ya Uongozi wa Mradi wa REGROW, inayojumuisha Makatibu wa Kuu wa Wizara mbalimbali nchini, Taasisi na Idara mbalimbali imekutana mkoani Morogoro kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi na kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.