Wadau waitikia wito wa wizara ya maliasili na utalii,makumbusho binafsi
21 December 2023, 08:09
Na mwandishi wetu,Iringa
Wadau wa Malikale nchini wameendelea kuitikia wito wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa kuanzisha Makumbusho binafsi ili kuhifadhi urithi wa Kihistoria wa Taasisi, Kabila au familia kwa maslai mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akifungua maonesho mapya kwenye Makumbusho ya Mkoa wa Iringa, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Mhifadhi Mkuu Idara ya Mambo ya Kale Bi. Prisca Kirway amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale, inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika uhifadhi wa utajiri mkubwa wa urithi wa kihistoria na Malikale nchini.
Bi. Kirway ameongeza kuwa Idara ya Mambo ya Kale inaendelea kuhamasisha wadau wa Malikale kuongeza mazao mapya ya Utalii nchini ili kuendana sambamba na matokeo chanya ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya The Royal Tour.
“Sera ya Malikale ya mwaka 2008 inatoa ruksa kwa jamii kubuni na kunzisha Makumbusho mbalimbali ili kurithisha mambo ya jamii zao” alisema Bi. Kirway
Aidha Bi. Kirway amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa wito kwa wadau na wananchi mbalimbali kujifunza kupitia Makumbusho ya Mkoa-Iringa na kuanzisha Makumbusho zao ili kurithisha tamaduni zao za masimulizi katika jamii zao.
Onesho jipya lililozinduliwa katika Makumbusho hiyo kupitia Program ya “Fahari Yetu” linaelezea masimulizi ya kusimumua kutoka katika jamii za mkoa wa Iringa na Njombe.