77% ya vijiji vimepata huduma ya maji safi na salama nchini
28 November 2023, 16:12
Na Hobokela Lwinga
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameitaka Sekta Binafsi kutumia fursa ya milango ya uwekezaji iliyofunguliwa na serikali ya awamu ya sita kuwekeza katika Sekta ya Maji. Wito huo ameutoa jijini Mbeya wakati akifungua kongamano la maji la mwaka 2023 lililoandaliwa na Jumuiya ya wasambazaji wa maji nchini (ATAWAS).
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa Sekta Binafsi katika kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi hivyo imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali kuhakikisha kunakuwepo na ustawi wa sekta hiyo.
Njia hizo ni pamoja na utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano kuanzia 2018 – 2023 wa namna ya kushirikisha sekta binafsi ambao umesaidia kuboresha Dawati la Ubia ngazi ya Wizara ambalo majukumu yake ni pamoja na kuratibu miradi ya ubia kati ya sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Amewashukuru wadau wote wa Sekta ya Maji kwa kusaidia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya serikali ambapo hadi sasa vijiji 9670 kati 12318 vilivyoko nchini Tanzania vimefikiwa na huduma ya majisafi na kufanya kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kufikia asilimia 77 wakati mijini huduma ikiwa imefikia asilimia 88.
Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa kongamano hilo Mwenyekiti wa Bodi ya ATAWAS Mhandisi Geofrey Hill amesema mkutano huo unafanyika kila mwaka ukilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji ili kupata suluhisho la upatikanaji wa majisafi na salama kwa watanzania. Ameshukuru ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka serikalini.
Kongamano la maji la mwaka 2023 limeandaliwa likiwa na kauli mbiu isemayo “PPP for Sustainable Water and Sanitation Services ” na limehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji nchini, Wakurugenzi wa Mashirika na Makampuni binafsi na Washirika wa Maendeleo.