Radi yaua mtu mmoja na Ng`ombe 27 Sumbawanga Rukwa
14 November 2023, 20:04
na Mwandishi wetu
Kufuatia Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha Maafa Wananchi wilayani sumbawanga Mkoani Rukwa wametakiwa kuchukua tahadhari za kiusalama ikiwa ni pamoja na kusimamisha Shughuli za Kilimo Pindi Mvua zinaponyesha.
Hayo yamejiri Mara baada ya Mvua kubwa iliyoambatana na Radi Kusababisha Maafa katika vijiji viwili tofauti wilayani humo ambapo Kijana mmoja aitwaye Edward Ibrahim Silungu mwenye Umri wa Miaka 32 katika Kijiji Cha Muze na Ng’ombe wawili aliokuwa akilimia Shambani kwake walifariki kwa kupigwa na radi, huku Katika kijiji cha Tamasenga Manispaa ya Sumbawanga Ng’ombe 25 wakifariki kwa kupigwa na radi
Akieleza Kuhusu tukio Hilo Shuhuda Ambaye ni Baba Mzazi wa Kijana huyo Ibrahim Silingu amesema kuwa walikuwa Shambani wakiendelea na Shughuli za Kilimo ndipo Mvua ilianza kunyesha Kisha baada ya Muda zilisikika Ngurumo zikiambatana na Radi na kusababisha Kijana wake kupigwa na Radi yeye pamoja na Ng’ombe wake wawili Wakati akiendelea na zoezi la Kulima Shambani kwake.
Akitoa Salamu za pole Kwa niaba ya Serikali Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe . Ally Chirukile ametoa wito Kwa wananchi kuchukua tafadhali katika kipindi hiki Cha Mvua kubwa ikiwa ni pamoja na Kuacha kufanya shughuli za Kilimo Kwa Kutumia Ng’ombe Wakati Mvua ikiendelea kunyesha.
Aidha amewataka wananchi wanaokaa sehemu za Mabonde kuhakikisha wanahamia sehemu amambazo ni Salama na kuzingatia utunzaji wa Mazingira inayosaidia miundombinu isiharibike Wakati wa Mvua kubwa.