Gari la kanisa laua wawili mchungaji akihamishwa Songwe
19 October 2023, 19:45
Kifo hakipigi hodi na hakuna anayeweza kuzui kifo ndio maana vitabu vya dini vina tusisitiza kujianda wakati kwa maana ya kutenda Mambo mema.
Na Ezekiel Kamanga
Watu wawili wamefariki kwa ajali ya lori namba T 644 AJC Mercedes Benz mali ya Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi baada ya kupinduka mtelemko wa Isalalo barabara ya Mbozi Msangano baada kufeli breki.
Taarifa za awali kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Theopista Mallya zimewataja waliofariki kuwa ni Levy Simkoko(30)aliyekuwa mzee wa Kanisa kutoka Ushirika wa Mbuga na Hosiana Gavu (21)ambaye ni mtoto wa mchungaji.
Aidha chanzo cha ajali kimetajwa kuwa ni kuharibika ghafla mfumo wa breki baada ya kupasuka bomba mbili za upepo hali iliyosababisha kwenda kasi na juhudi za dereva zikashindikana kisha kupinduka na kusababisha vifo viwili na majeruhi wawili ambao wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Imedaiwa lori lilikuwa na watu kumi na mbili ambao walikuwa wanamsindikiza mchungaji Emmanuel Gavu aliyehamishwa kutoka Ushirika wa Mbuga kwenda Ushirika wa Msangano.
Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi Mchungaji Laurence Nzowa ambaye yupo safarini Jimbo la Rukwa amesema uhamisho huo ni wa kawaida na ametoa pole kwa familia na Kanisa kwa ujumla.
Katibu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi Mchungaji Rayson Kibona amesema baada ya kupata taarifa ya ajali walifika eneo la tukio na kuwafikisha majeruhi hospitali.
Miili ya marehemu ilihifadhiwa hospitali na taratibu zote za mazishi zimefanywa na Kanisa na wote wamepumzishwa.
Katibu amesema msiba huu ni pigo kwa Kanisa na ametoa pole kwa familia na waumini wote wa Kanisa la Moravian Tanzania sanjari na kuwashukuru wale wote walifanikisha hatua zote mpaka mazishi.
“Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina la Bwana lihimidiwe amina”