Tupo tayari kuboresha utalii nchini -REGROW
14 September 2023, 20:00
Wahenga wanasema jasiri haachi asili hivyo ndivyo unaweza kusema kutokana na kile ambacho kimekuwa kikifanywa na wizara ya maliasili na utalii nchini Tanzania kutokana na kudumisha mila na destri ya mtanzania hasa katika kuenzi ngoma za asili na vyakula kwa kila kabila.
Na Moses Mbwambo
Wizara ya Maliasili na Utalii nchini kupitia mradi wa Kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii Nyanda za juu Kusini (REGROW) imechagiza uanzishwaji wa vikundi vya kijamii vilivyoanzisha mazao mapya ya Utalii kama vile ngoma za asili,vyakula vya asili, bidhaa za kiutamaduni kwa lengo la kuinua wananchi kiuchumi pamoja na ulinzi wa Maliasili nchini.
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi wa jamii ya Kabila la Kimasai, vinavyowezeshwa na Mradi wa REGROW, Bw. Madicini Matayani, amesema Watalii wanapoenda au kutoka katika Hifadhi ya Taifa Ruaha wanapitia kwenye vikundi vyao na kufurahia Utalii wa kiutamaduni hususani ngoma, nyama inayochomwa kiasili, Mavazi ya asili nk.
Bw. Matayani ameongeza kuwa kutokana na fedha wanazozipata kutoka kwa Watalii maisha ya familia zao yamebadilika na sasa wanamiliki nyumba za kisasa, wanasomesha watoto, wananunua chakula cha uhakika na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Wanufaika wengine wa Mradi kutoka Kikundi cha Tembo Pilipili kijijini hapo wameeleza kufurahishwa na mradi huo kwani kwasasa wameweza kusaidia kuimarisha shughuli za uhifadhi pamoja na kuwa marafiki wa Wanyamapori kwa kuandaa njia rafiki za kudhibiti Tembo kuingia katika makazi ya watu na kuharibu mazao yao kupitia mbinu za asili.
Akizungumzia Mradi huo, Naibu Msimamizi wa Mradi wa REGROW, Bi. Blanka Tengia amebainisha kuwa, mradi huo unatekelezwa kwenye Hifadhi nne, ambazo ni Hifadhi ya Taifa Ruaha, Hifadhi ya Taifa Nyerere, Hifadhi ya Taifa Mikumi na Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa na kuwa REGROW umekusudia kuimarisha uhifadhi wa Ikolojia na kuwezesha jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.