Wananchi Mbeya wahimizwa kutunza mazingira kuongeza uzalishaji wa maji
13 September 2023, 13:38
Maisha ya binadamu yeyote duniani kote yanategemea mazingira na mtunzaji wa mazingira ni binadamu mwenyewe hivyo basi ni wajibu kutunza mazingira ili kuepukana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Na Hobokela Lwinga
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa- 2023 Abdullah Shaib Kaim ameipongeza Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa kwa kuendelea kulinda na kuhifadhi chanzo mto Nzovwe kwa kupanda miti 490 ambayo ni rafiki wa mazingira.
Pongezi hizo amezitoa baada ya mwenge wa uhuru kutembelea chanzo hicho chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 29 kwa siku na kujionea namna ambavyo uzalishaji wa maji unafanyika.
Kwa upande wake mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi(Mb), Naibu Waziri wa Maji amewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya vyanzo vya maji kuendelea kutunza na kulinda ili kuhakikisha huduma za maji zinakuwa endelevu kwao.
Naibu Waziri huyo amesema serikali kwa mwaka huu wa fedha imeendelea kutekeleza mradi wa maji wa Mto Kiwira ambao unagharimu shilingi bilioni 117 ambapo mpaka sasa shilingi bilioni 14.9 zimetolewa ikiwa ni malipo ya awali ya mkandarasi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ameishukru serikali kwa utekelezaji wa miradi ya maji ndani Jiji la Mbeya.
Chanzo cha Maji cha Ivumwe (mto Nzovwe)kinahudumia wakazi wa mitaa ya Forest Mpya, Forest ya Zamani, Mwanjelwa, Old Airport, Iyela, Iyunga, Iwambi, Viwanda vya Coca-Cola, pamoja na Veta.