Baraka FM
Baraka FM
15 November 2025, 08:15

Kutokana na uzembe wa madereba barabara ajali zimezidi kukatisha uhai wa watu wengi
Na Ezekiel Kamanga
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Agustino Senga, amethibitisha kutokea kwa ajali mbaya ya barabarani iliyoua mtu mmoja na kuharibu magari mawili. Ajali hiyo imetokea saa 1:00 asubuhi ya Novemba 14, 2025, katika eneo la Senjele, Wilaya ya Mbozi, barabara kuu ya Tunduma–Mbeya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na SACP Senga, ajali hiyo ilihusisha gari aina ya FAW Lori lenye namba T.717DWD/T.847DQT mali ya Midwest Minerals Ltd, ambalo lilikuwa likitoka Tunduma kuelekea Mbeya. Lori hilo liligongana uso kwa uso na gari la Toyota Land Cruiser, namba SU.43390, mali ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Katika ajali hiyo, dereva wa NIMR, Azza Kamendu (39), Mkazi wa Mbeya, alifariki dunia papo hapo. Magari yote mawili yaliharibika vibaya.

Kamanda Senga amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali ni dereva wa lori la FAW kufanya “wrong overtaking”, yaani kujaribu kupita magari mengine katika eneo hatarishi bila tahadhari, hatua iliyosababisha kugongana uso kwa uso.
Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali kumtafuta dereva wa lori hilo, ambaye alikimbia mara baada ya ajali na hadi sasa hajapatikana.

Kamanda Senga ametumia nafasi hiyo kuwataka madereva kuzingatia sheria, alama na michoro ya barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.