Baraka FM
Baraka FM
18 June 2025, 13:13

Sheria ni msumeno huwa unakata kote kote kauli hii ina maana kuwa hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria.
Na Hobokela Lwinga
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Emilian Joseph Duzu (21), kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzake Gerald Philbert Said (22) ambaye alikuwa mwaka wa tatu chuoni hapo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo limetokea Juni 14, 2025 majira ya saa 11:00 alfajiri katika klabu ya burudani iitwayo Mbeya Pazuri iliyopo Jijini Mbeya, ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimmjeruhi marehemu kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali tumboni.

Gerald alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu, lakini alifariki dunia saa 7:00 mchana siku hiyo hiyo kutokana na majeraha aliyopata.Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa Polisi, chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na ulevi wa kupindukia wakiwa ndani ya klabu hiyo.
Inadaiwa kuwa walinzi wa klabu (mabaunsa) waliingilia kati na kuwaamuru watoke nje, lakini mtuhumiwa alikwenda eneo la maegesho ya magari ambapo marehemu alimfuata na ndipo alipopata jeraha hilo hatari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga ametoa wito kwa wananchi, hususan wanafunzi, kujiepusha na matumizi ya pombe kupita kiasi na vitendo vyovyote vya kihalifu, akisema kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya wale wote wanaokiuka taratibu za usalama.
Aidha, Jeshi hilo limewaasa wanafunzi wote mkoani humo kuzingatia masomo yao na kutumia muda wao kwa njia chanya ili kuepusha matukio yanayoweza kuhatarisha maisha yao na mustakabali wao wa kielimu.