Baraka FM

Jeshi la Polisi Mbeya lapokea vitendea kazi

30 March 2025, 17:34

RPC Mkoa wa Mbeya katikati akipokea kompyuta (Picha na Hobokela Lwinga)

Katika kurahisisha utendajikazi katika Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamati ya Usalama Barabarani imekabidhi kompyuta kwa jeshi hilo.

Na Hobokela Lwinga

Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya yakabidhi vitendea kazi vya ofisi kompyuta na “Photocopy Machine” kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza Machi 29, 2025 katika uwanja wa mazoezi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mbeya baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoani humo Mhandisi Rajabu Ghuliku amesema kuwa msaada huo unalenga kurahisisha utendaji kazi na kuleta ufanisi katika jitihada za kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.

Mhandisi Rajabu Ghuliku(kushoto) akikabidhi kompyuta

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewataka Wakuu wa Polisi Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya kutunza vitendea kazi hivyo na kuhakikisha vinatumika vizuri ili kuleta matokeo chanya katika kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga

Aidha, Kamanda Kuzaga ameishukuru Kamati hiyo kwa vitendea kazi hivyo kwani kutokana na ukuaji wa matumizi ya TEHAMA ikiwemo mifumo ya kidigitali ya utendaji kazi ndani ya Jeshi la Polisi ni wazi kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuongeza tija na weledi katika utendaji kazi.

Naye, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoani Mbeya ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoa, SP Notker Kilewa amesema kuwa msaada huo unakwenda kuongeza weledi katika utendaji kazi za kikosi hicho na kutoa shukrani kwa kamati kuweza kutoa kompyuta za mezani saba na “heavy duty photocopy machine” moja.

Vifaa vyilivyo pokelewa na jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya