Barabara ya Mbalizi-Shigamba kupendwa kwa shilingi bilioni 2
30 July 2024, 18:53
Barabara ni kiunganishi kikubwa cha maendeleo ya nchi na watu, ukosefu wa miundombinu hiyo husababisha watu kushindwa kuzalisha na kupata uchumi Mara nyingine hata kukosa huduma Bora za afya hasa pindi mama majamzito anapokwenda kujifungua .
Na Josea Sinkala, Mbeya
Wakala wa Ujenzi wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya umesema unatarajia kuanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbalizi hadi Shigamba Umalila kwani tayari fedha za kuanzia zimetolewa shilingi billion mbili.
Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa ujenzi wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya Mhandisi Kamokene Sanke wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sanje kata ya Santilya wilayani Mbeya kwenye ziara ya Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza kusikiliza kero za wananchi.
Amesema Serikali kuu chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha Billion mbili za awali ili kuanza ujenzi wa barabara ya lami ya Mbalizi Shigamba (Km 52) na kwamba ujenzi huo unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
“Mheshimiwa Rais tayari ametoa fedha shilingi Billion mbili na sasa tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi ili kuanza utekelezwaji wa mradi wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami”, amesema Mhandisi Sanke, Kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya na kuwaomba wananchi kuendelea kujenga imani na viongozi wao kuwa barabara hiyo itajengwa.
Naye Arcad Tesha kaimu meneja wa Wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA wilaya ya Mbeya, amesema barabara inayoanzia njiapanda ya Soweto hadi Sanje ina urefu wa kilomita nane na kwa kuanza kuanzia juma lijalo wataanza kuweka kifusi kwenye eneo la kilomita tatu za barabara hiyo.
Pia TARURA wilaya ya Mbeya inaelekeza nguvu kwenye ujenzi wa daraja linalounganisha vijiji vya Sanje na Itizi kutokana na daraja hilo kutopitika na kuhusu barabara nyingine iliyolalamikiwa amesema haipo kwenye mfumo wa mtandao wa barabara na pamoja na hayo TARURA haitanyamaza.
Pia barabara ya Itizi Sanje Jojo yenye urefu wa kilomita 15 imeelezwa kuwa ni kero hivyo TARURA imeeleza kuishughulikia kuhakikisha inapitika.
Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amesisitiza wataalam wa barabara mjini na vijijini (TARURA) kutimiza matakwa hayo ya wananchi ili kuwasaidia kutokana na kutokuwa na miundombinu rafiki ombi ambalo pia amelielekeza kwa wahandisi wa maji kiu yake kuu ikiwa ni kuona wananchi wake wanapata huduma ya maji safi.
Kwa upande wake Beatrice Keffa Urio ambaye ni ofisa kutoka ofisi ya mipango Halmashauri ya Mbeya, amesema kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwa Serikali ipo ili kuwatumikia wananchi hivyo wataendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa maendeleo ya wananchi.