Baraka FM

Dkt. Tulia akabidhi nyumba kwa mahitaji Mlimba, Morogoro

26 July 2024, 21:48

Wahenga wanasema kutoa ni moyo si utajiri hii inatukumbusha kuwa kila mtu anawajibu wa kumsaidia mahitaji yeyote popote anapokutana nae haijalishi ni mhitaji wa mahitaji gani.

Na Ezekiel Kamanga

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson amekabidhi nyumba, madaftari, kiti mwendo kwa wahitaji na marumaru kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi kata ya Ching’anda almashauri ya Mlimba wilaya ya Kilombero.

Awali Dkt Tulia Ackson amekabidhi kiti mwendo kwa Catherine pia madaftari kwa watoto wanaoishi mazingira magumu na malumalu makasha arobaini kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Ching’anda.

Dkt Tulia Ackson ametoa wito kwa wadau wengine kuungana na Taasisi yake ili kuwasaidia watu wenye uhitaji kwani Taasisi haiwezi kuwafikia watu wote.

“Hata kama wawezi kujenga nyumba lakini wanaweza hata kununua madaftari kwa watoto”alisema Dkt Tulia.

Spika Tulia akikabidhi vifaa vya shule

Baada ya kukabidhi vifaa vivyo Dkt Tulia amekabidhi nyumba kwa Ambalile Mwala Mkazi wa Kitongoji cha Matankini Kijiji cha Ching’anda Kata ya Ching’anda.

Akitoa taarifa kwa wananchi wa Ching’anda Afisa Habari wa Taasisi ya Tulia Trust Joshua Mwakanolo amesema walibaini uhitaji wa Mzee Ambalile Mwala kupitia mitandao ya kijamii ndipo walipofika kuanza ujenzi kutokana na maelekezo ya Spika wa Bunge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust.

“Kiu yangu ni kuona watu wanatabasamu”alisema Dkt Tulia.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba Godfrey Kunambi amemshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson kwa kumsaidia mwananchi wake jambo alilolifanya ni matendo ya huruma.

Kwa upande wake Mzee Ambalile Mwala amemshukuru Dkt Tulia Ackson kwa jinsi alivyoguswa kwake hatimaye kumjengea nyumba kwani alikuwa akifukuzwa katika nyumba mbalimbali alizokuwa akipanga kutokana na changamoto za maisha.

Wananchi wakifurahia ujio wa spika Tulia kwenye eneo lao

“Naona huu ni muujiza kwangu awali niliona kama ndoto na sikuamini nilipofikiwa na vijana wake kwa ajili ya ujenzi “alisema Ambalile huku akibubujikwa na machozi ya furaha.