Watu wenye ulemavu Rungwe wapewa tabasamu na kanisa la Moravian
6 July 2024, 22:02
Si mara ya kwanza kwa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini kugawa msaada wa viti mwendo kwa watu wenye ulemavu, ambapo tangu kuanza kwa mradi huu zaidi ya watu 50 wamenufaika na wengine wakiendelea kuibuliwa.
Na mwandishi wetu
Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini limegawa Viti mwendo kwa watu wenye ulemavu Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya.
Tukio hilo la ugawaji viti mwendo kwa watu wenye ulemavu limefanyika siku ya Ijumaa katika ukumbi wa Moravian Hostel Tukuyu na kuhudhuriwa na Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Rungwe Ndg. Yohana Kibona.
Msaada huo wa viti mwendo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni sita, umetolewa kupitia mradi wa kuwasaidia watu wenye ulemavu kupitia kampeni ya Usiwaache Nyuma Project inayoendeshwa na Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini kwa ufadhili wa shirika la Mission 21 .
Akizungumza na baada ya ugawaji wa viti hivyo, kwa niaba ya uongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini, Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Edger Teacher Mwabungulu , amewashukuru sana wafadhili kutoka Shirika la Mission 21 na wengine wanaounga mkono jitihada za kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma.
Pia ametoa wito kwa jamii kujitolea kuunga mkono jitihada hizo za kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuchangia kile walichonacho ili kufanikisha jitihada hizo.
Wadau wengine walioshiriki tukio hili ni shirika la Tulia Trust ambao kwa upande wao wamelipongeza Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini na kuahidi kushirikiana nao katika kuwawezesha watu wenye ulemavu.