Kanisa la Moravian lamuomboleza mama mchungaji Sabina Mwakilembe
6 July 2024, 20:18
Hatimaye mwili wa Marehemu Sabina Mwakilembe mke wa Mchungaji mstaafu Marehemu Amosi Mwasambapa umezikwa katika makaburi ya familia eneo la kalobe jijini Mbeya.
Na Hobokela Lwinga
Askofu wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini Magharibi Robert Pangani ameiasa jamii kuishi maisha Matakatifu ya kumpendeza Mungu nyakati zote kwani hakuna mtu anajua siku ya kufa hapa duniani.
Wito huo ameutoa wakati wa Ibada ya kuagwa Marehemu Sabina Joseph Mwakilembe mke wa mchungaji mstaafu Marehemu Amosi Mwasambapa katika kanisa la Moravian Ushirika wa nzovwe jijini Mbeya.
Nae katibu Mkuu wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la kusini magharibi Ndugu Israeli Mwakilasa na mwenyekiti wa wilaya ya Mbalizi mchungaji Erika Mwanijembe wamesema kama kanisa wamepoteza mtu muhimu kutokana na utumishi ambao alikuwa nao katika kanisa hasa katika idara ya umoja wa wanawake ushirikani Nzovwe sambamba na kwaya kuu.
Kwa upande wake mwenyekiti Wa kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mbozi mkoani Songwe mchungaji Lawrence Nzowa amesema wakati akiwa mchungaji katika Ushirika huo Marehemu alikuwa mshauri mkubwa yeye na familia yake.
Hata hivyo mchungaji wa Ushirika wa Nzovwe Jonamu Msangawale ameeleza namna ambavyo marehemu alivyotwaliwa kuwa walikuwa nae katika ibada ya akina mama majira ya asubuhi kabla ya umauti kumfika majira ya mchana,huku mchungaji mstaafu profesa Nkaisule Nzowa ameshauri kila muumini kusimama imara kumtumikia Mungu.
Marehemu Sabina Mwakilembe alizaliwa January 25,1961 na ametwaliwa Julai 3,2024 katika hospitali ya Rufaa mkoa wa Mbeya ambako alikuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.