Baraka FM

kambi ya SKAUT yafungwa Songwe

26 June 2024, 12:39

Kambi ya Vijana wa SKAUT ngazi ya Mkoa katika mkoa wa songwe imetoa matokeo chanya kwa vijana washiriki mkoni Songwe.

Na mwandishi wetu,Songwe

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Ester Mahawe, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, amehitimisha mafunzo ya kambi ya vijana wa SKAUT ngazi ya Mkoa yaliyofanyika kwa muda wa siku nne na kuhitimishwa leo, tarehe 25 Juni, 2024, katika Wilaya ya Mbozi. Vijana 137 walishiriki mafunzo haya kutoka wilaya zote za mkoa wa Songwe.

Mhe. Mahawe amewapongeza vijana kwa uzalendo wao waliouonesha kwa kushiriki mafunzo hayo. Alisema, “Niwapongeze sana kwa kujitoa kwenu kuja katika kambi hii. Wako vijana wengi katika mkoa wetu lakini kwanini nyie? Ni kwasababu ya uzalendo mkubwa mlionao dhidi ya nchi yenu.”

Aidha, Mhe. Mahawe amewataka vijana hao kuweka mafunzo yote waliyojifunza katika vitendo ili kusaidia mkoa wa Songwe na taifa kwa ujumla. Pia aliwasisitizia kujiandaa na kambi kubwa ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro.

Kwa siku walizoshiriki mafunzo hayo, vijana walitembelewa na taasisi mbalimbali za mkoa wa Songwe ikiwa ni pamoja na TAKUKURU na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe.