Rais Samia mgeni rasmi wakfu wa askofu mteule Moravian
17 April 2024, 21:17
Taasisi za dini ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa mchango mkubwa wa kutunza, kulinda amani ya taifa hali hiyo inathibitishwa na maridhiano yaliyopo baina ya taasisi za dini pamoja na serikali.
Na Hobokela Lwinga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ibada ya kumuweka wakfu na kumuingiza kazini askofu mteule wa Kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kusini Magharibi Mbeya Mch.Robert Pangani.
Akizungumza na vyombo vya habari makao makuu ya jimbo hilo Makamu Askofu wa kanisa hilo Kenani Panja amesema ibada ya wakfu itafanyika Juni 2, 2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu Teofilo Kisanji cha kanisa la Moravian Tanzania kilichopo jijini Mbeya.
Askofu Panja amesema mbali na wakfu wa kiongozi huyo, viongozi wa kanisa, maaskofu, wachungaji pamoja na waumini watafanya maombi kwa ajili ya kumwombea Rais kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuongoza nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kusini Magharibi Ndg. Israel Mwakilasa amesema tukio hilo litaambatana na utoaji wa tuzo kwa baadhi ya washiriki lengo likiwa ni kutambua mchango wao katika kanisa huku akisema ibada hiyo itahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wa dini na madhehebu ya ndani na nje ya nchi.
Ibada Takatifu ya wakfu ya askofu mteule mchungaji Robert Pangani inafuatiwa kuchaguliwa kwake na mkutano mkuu Novemba 02, 2023 ushirikani Ruanda kutokana na kustaafu kwa aliyekuwa askofu wake Dkt. Alinikisa.