Wakristo watakiwa kuchangia damu kusaidia wagonjwa wenye uhitaji
16 April 2024, 15:28
Jamiii imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha banki ya damu kuwa na akiba ya kutosha.
Na Anna Mbwilo
Waumini wa kanisa la TAG Nzovwe jijini Mbeya wametakiwa kuchangia damu kwa lengo la kuiwezesha benki ya damu kuwa na akiba ya kutosha ili kusaidia watu mbalimbali wanaohitaji kuongezewa huduma hiyo.
Hayo yamesemwa na Mchungaji wa kanisa hilo Pasco Masawili wakati akizungumzia umuhimu wa kuchangia damu katika kuelekea maadhimisho ya miaka 85 ya kanisa la TAG nchini na miaka 51 ya kanisa la TAG Nzovwe.
Mch. Masawili amesema kuwa zoezi la uchangiaji damu ni sehemu ya kuwasaidia wahitaji kwa kuwa suala hilo ni la kiroho na kiimani.
Nae katibu wa kanisa hilo Aggyley Nzingana amesema wameamua kuungana pamoja kuchangia damu kwa lengo la kuigusa jamii huku akiwashukuru waumini kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo.
Kwa upande wao baadhi ya waumini wa kanisa hilo wameeleza kufurahishwa na hatua ya wao kuchangia damu huku wakiushukuru uongozi wa kanisa kwa kuwahamasisha kuchangia damu ili kusaidia jamii.
Hata hivyo mratibu wa huduma za maabara jiji la Mbeya Elia Isaya ameushukuru uongozi wa kanisa la TAG Nzovwe kwa kuchangia damu huku akiwataka wananchi kuachana na Imani potofu kuhusu uchangiaji damu.