Mlima Kawetere wameguka, mifugo yapotea, nyumba zabomoka
14 April 2024, 20:34
Wakati mvua zikiendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kasababisha madhara kwenye jamii, hali hiyo sasa imeukumba mkoa wa Mbeya baada ya mvua kunyesha na kusababisha mlima kumeguka na tope lake kuzingira makazi ya watu.
Na Josea Sinkala,Mbeya
Zaidi ya nyumba ishirini za makazi zimebomoka na kusababisha zaidi ya watu 200 kukosa makazi kutokana na kuzuka kwa maporomoko ya tope katika Mlima Kawetele kata ya Itezi Uyole jijini Mbeya.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aprili 14, 2024 na kugusa makazi hayo ya mitaa miwili ya Mwasote na Gombe Kaskazini kata ya Itezi Uyole ambapo ni kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia April 14 iliyosababisha huzuni kwa baadhi ya wananchi wa maeneo hayo.
Wakazi hao wanasema walikumbwa na kadhia hiyo baada ya mlima Kawetele kumeguka na kuleta mafuriko ya tope hali iliyosababisha athari kwao hususani ya mazao kuharibiwa pamoja na mifugo kadhaa na kubomolewa kwa nyumba zao zilizofukiwa na matope sanjari na samani za ndani.
Mashuhuda na waathirika wa mafuriko hayo wanasema mafuriko hayo yalianza dalili majira ya saa saba usiku lakini mapema alfajiri majira ya saa 11 hadi saa 12 asubuhi zilianza dalili za matope kushuka ndipo baadaye matope mengi yalianza kushuka kutoka kwenye mlima huo (Kawetere).
Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya Mrakibu wa Zimamoto Marumbo Ngata, udongo huo umeporomoka kutoka eneo la katikati ya mlima Kawetele hadi kwenye makazi ya watu akizitaja shughuli za kibinadamu kuwa ndizo zimesababisha udongo wa mlima huo kulegea na kuwa rahisi kusombwa na maji.
Mpaka sasa hakuna madhara kwa binadamu licha ya kaya zaidi ya ishirini kukosa makazi na tayari wakazi wa eneo hilo lililoathirika wamehamisha familia zao kuzipeleka sehemu salama.
Diwani wa kata ya Itezi Mhe. Sambwee Shitambala amesema maafa hayo yanachochewa na Serikali ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambayo imekuwa ikipima viwanja hadi maeneo ya hatari kama hayo ikiwa ni pamoja na kuruhusu shughuli za kilimo pembeni mwa mito na milimani.
Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mbeya Mhe. Beno Malisa, amesema licha ya kaya kuathirika lakini pia kuna shule imezama kwenye tope upande mmoja na tayari wamechukua hatua za haraka za kuwahamisha wanafunzi zaidi ya 250 na Jeshi la Zimamoto lipo eneo la tukio likiendelea kutoa msaada.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zubery Homera, amefika eneo la tukio na kuonya watumishi wa Ardhi Jiji la Mbeya kuacha tabia ya kupima viwanja maeneo hatarishi na kuelekeza Halmashauri ya Jiji kuhakikisha waathirika wanawekwa kwenye mazingira rafiki wakati jitihada zingine zinaendelea, maelekezo ambayo yamepokelewa na halmashauri kupitia mstahiki Meya wa Jiji Dourh Mohammed Issa.