Dkt. Tulia akabidhi nyumba, azindua kiwanda cha nafaka, atembelea athari za mafuriko Igawilo
11 April 2024, 16:18
Dkt Tulia amewataka wananchi na watu wenye unafuu wa maisha kuwagusa watu wenye uhitaji kila mmoja Kwa namna alivyojaliwa badala ya kubeza wale wanaotoa misaada kwenye jamii.
Na Ezekiel Kamanga
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tulia Trust Mhe. Dkt. Tulia Ackson amekabidhi nyumba Kwa Singwava Jackson mkazi wa mtaa wa ltanji Kata ya Iganjo Jijini Mbeya mjane mwenye watoto sita baada ya kuishi kwenye nyumba ya maturubai Kwa zaidi ya miaka minne.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi,Seikali,Viongozi wa Dini,viongozi wa Mila na wananchi ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera.
Katika hotuba yake Dkt Tulia amewashukuru wananchi Kwa namna walivyoguswa kuungana na taasisi yake kuhakikisha mama huyo anaishi vizuri yeye na familia yake.
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya Patrick Mwalunenge amempongeza Dkt Tulia Kwa kuwagusa watu wenye uhitaji kwani hiyo ni sadaka mbele za Mungu.
Ametoa wito kwa wana CCM kuwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 mgombea Urais ni Dkt Samia Suluhu Hassan na Ubunge wa Mbeya mjini ni Dkt Tulia Ackson kwani kazi walizozifanya zinaonekana kwa macho.
Mwalunenge amechangia shilingi laki tano ili ziweze kumsaidia mjane huyo na familia yake pamoja na mahitaji ya shule kwa watoto.
Naye Mjumbe wa mkutano Mkuu Taifa(NEC)Ndele Mwaselela amesema yeyote anayetaka kugombea Ubunge Jimbo la Mbeya mjini aanze kutoa misaada sasa na ajipime kama anatosha nafasi hiyo.
“Mimi siyo mnafiki na siogopi kusema ukweli kwamba tutaimarisha ulinzi Kwa Dkt Tulia”alisema Mwaselela.
Hata hivyo Mwaselela amechangia shilingi laki tano Kwa ajili ya kuongeza mtaji na mahitaji kwa familia hiyo.
Beno Malisa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera amesema Dkt Tulia amefanya mambo mengi katika Jiji la Mbeya kama ujenzi wa madarasa,zahanati,bima kwa wazee,mitaji kwa wana wake,sare za shule ,mikopo ya pikipiki na Bajaj.
Naye Sheikh Ibrahim Bombo kwa niaba ya Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Ayasi Njalambaha amesema Dkt Tulia amekuwa akitoa misaada bila kujali itikadi za kidini na kisiasa.
Chifu Roketi Mwanshinga ni mmoja wa watu waliohudhuria hafla hiyo huku akiwataka wananchi kushikamana kumuunga mkono Dkt Tulia kwa maendeleo ya Mbeya naye akichangia sukari Kwa familia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa ltanji Kata ya Iganjo Jaivah Washaha mbali ya kumshukuru Dkt Tulia kufanikisha ujenzi wa nyumba ya mwananchi wake naye ameunga mkono kwa kuingiza maji kwa mjane sanjari na kuchangia pango la nyumba ujenzi ulipokuwa unaendelea.
Mbali ya kukabidhi nyumba Dkt Tulia amekabidhi pia fedha taslim zaidi ya shilingi milioni tatu na laki sita ili kumsaidia kuongeza mtaji na mahitaji ya shule kwa watoto pia mahitaji ya ndani.
Wadau mbalimbali wameipamba hafla hiyo wakiwemo wafanyabiashara na makada wa chama ambao walitoa vyakula,godolo,jiko la gesi,nguo na samani hali iliyoleta tabasamu kwa mama huyo.
Akiongea huku akibubujikwa machozi Singwava Jackson amemshukuru Dkt Tulia kwa kuisitiri familia yake kwani alikuwa akiishi kwenye turubai kwa hofu hasa mvua zilipokuwa zikinyesha na pia hakuwa na mtaji.
Awali Dkt Tulia ametembelea eneo la Igawilo lililokumbwa na mafuriko na kuwapa pole wananchi waliokuwa wakizibua mifereji ili kuepusha mafuriko.
Dkt Tulia amehitimisha ziara yake kwa kuzindua kiwanda cha kusaga na kukoboa nafaka kilichopo Igawilo ambapo amechangia mtaji wa shilingi milioni moja ili waweze kununua nafaka.
Mwenyekiti Selina Mbeyale kwa niaba ya kikundi mbali ya kushukuru kupokea fedha amesema mashine hazifanyi kazi kwa ufanisi kutokana na ukosefu wa mtaji,wateja na changamoto ya kukatika kwa umeme.
Dkt Tulia amemuagiza Diwani wa Viti Maalum Jiji la Mbeya Attu Msai kuhakikisha anawasimamia wajane hao ili mashine ziweze kufanya kazi kwa ufanisi ili kukamilisha marejesho ya mkopo wa Jiji wanaodaiwa zaidi ya shilingi milioni mbili