Waandishi wa habari watakiwa kuelimisha jamii
29 February 2024, 16:58
Na Mwandishi wetu Songwe
Kamanda wa Polisi mkoani Songwe SACP Theopista Mallya amewataka waandishi wa habari mkoani hapa kuendelea kuielimisha jamii dhidi ya vitendo vya ukatili.
Kamanda Mallya ameyasema hayo February 28, mwaka huu, mbele ya viongozi wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani hapa waliofika ofisini kwake kumpongeza kufuatia kupandishwa cheo kutoka Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP na kuwa Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP.
Amesema pamoja na kupongezwa kwa hatua ya kupandishwa cheo, lakini si mafanikio yake, bali ni kwa askari wote wa Mkoa wa Songwe, Wananchi wanaochukia uhalifu na Waandishi wa habari ambao kwa kiasi kikubwa wanaelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo maswala ya ukatili.
“Vitendo vya ukatili kwa ujumla wake ni vitendo vibaya ambavyo vinasababisha wanaofanyiwa kuamua kujiua, unakuta mtoto mdogo anafanya maamuzi kama hayo ambayo ukifuatilia nyuma yake kuna ukatili uliofanyika” amesema SACP. Mallya
Ameongeza kuwa vyombo vya habari viendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu ukatili na mwisho wa siku watu wote wataelimika na kuacha ukatili.
Pamoja na Pongezi hizo Kamanda Mallya alikabidhiwa Cheti cha kutambua mchango wake kwa kuelimisha jamii na Mwenyekiti wa umoja wa waandishi wa habari Mkoni humo Bw. Stephano Simbeye
Awali Bw. Simbeye amesema uamuzi wa kumpongeza kamanda Mallya ni matokeo ya makongamano ya majadiliano yaliyofanyika mwaka Jana baina ya Polisi na waandishi wa habari.
“Tumeamua kuja hapa kwako Kamanda Ili tukupongeze kufuatia kupandishwa cheo na kuwa tunaamini haya ni mafanikio yako binafsi lakini pia inatokana na ushirikiano wa wananchi wote wa Songwe.