RC Dendego amwagiza DED manispaa ya Iringa kutenga eneo ujenzi wa mahakama
1 February 2024, 22:39
Na Moses Mbwambo, Iringa
Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego ameuagiza Uongozi wa Manispaa ya Iringa kutenga eneo jipya kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama baada ya majengo ya mahakama yaliyopo kuonekana eneo lake limebanana.
Mhe. Dendego ameyasema hayo hayo wakati wa kilele cha siku ya sheria kilichofanyika mjini Iringa ambapo amesema kuwa moja ya changamoto aliyoipokea ni kubanana kwa jengo hilo hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhakikisha anatafuta eneo kubwa lenye uwazi kwaajili ya ujenzi wa Mahakama Kuu.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Jaji Alvis Mugeta ametoa shukurani kwa Mkuu wa Mkoa kwa maagizo aliyoyatoa na kusema kuwa kwa mwaka huu mpya wa Kimahakama Mahakama hiyo itaendelea kutenda haki na kuhakikisha kesi ambazo hazina ulazima wa kuchukua muda mrefu zinashughulikia kwa mujibu wa sheria.
Hivi sasa majengo ya mahakama Kuu, ya mkoa na ile ya wilaya yanapakana na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa pamoja na magereza ya mkoa huo na hivyo kusababisha msongamano wa huduma na muingiliano usio na afya kwa jamii.