Mwalimu mbaroni kwa tuhuma za unyang’anyi Mbeya
26 January 2024, 21:45
Na mwandishi wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu akiwemo Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwaselela Azimio Gerald [31] Mkazi wa ZZK mji mdogo wa Mbalizi na wenzake wawili Furaha Issa [32] na Goodluck Mwakajisi [25] wote wakazi wa Iwambi kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha, uporaji, uvunjaji wa nyumba, maduka na wizi.
Akizungumza Januari 26, 2024 na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga ameeleza kuwa watuhumiwa walikamatwa Januari 25, 2024 katika misako iliyofanyika maeneo mbalimbali ya Mji mdogo wa Mbalizi.
Kamanda Kuzaga ametaja baadhi ya mali za wizi walizokutwa nazo watuhumiwa ikiwemo Television 2, redio Subwoofer 3, redio ndogo 4 na Spika zake, Laptop 8, simu za mkononi 16 pamoja na mashine moja ya kupimia damu.
Ameongeza kuwa, watuhumiwa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia nyumba na maduka, visu 4, mapanga 3.Baadhi ya mali zimetambuliwa na wahanga.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kufika kituo cha Polisi Mbalizi kwa ajili ya kutambua mali zao.