Serikali imetenga bilioni 48 mikopo ya Wanafunzi ngazi ya stashahada kwa mwaka wa fedha 2023/2024
16 January 2024, 21:22
Na Hobokela Lwinga
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa masomo wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada.
Amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Chuo Kikuu Katoliki Mbeya (CUoM) mkoani Mbeya na kueleza kuwa mpango huo, ambao ni maono na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unalenga kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kuwezesha wahitimu wa vyuo nchini kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na kimataifa.
“Lengo lingine la Rais Dkt. Samia ni kuona vijana wengi wanapata elimu itakayowapa ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Taifa,” amesema.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa Serikali imetenga Dola za Kimarekani milioni 1 kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambazo zinasomesha wahadhiri 27 kutoka vyuo vikuu visivyo vya Serikali.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa fedha hizo pia zitatumika kugharamia wahadhiri saba katika ngazi ya Shahada ya Umahiri na 20 katika Shahada ya Uzamivu kwa programu za afya na sayansi shirikishi.