Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi kwa kutoa vitendea kazi
16 January 2024, 14:34
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe.Benno Malisa ameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha linapata vitendea kazi ikiwemo magari kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi.
Ametoa kauli hiyo wakati akikabidhi magari mapya matatu kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga ikiwa ni sehemu ya mgao uliotolewa na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura.
Mhe.Malisa amepongeza jitihada za Jeshi la Polisi katika kuzuia na kupambana na uhalifu ikiwemo utekelezaji wa falsafa ya Polisi Jamii ambayo imekuwa chachu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura kwa kutoa magari hayo ambayo yanakwenda kuimarisha doria za barabara kuu na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Aidha ameeleza kuwa magari hayo ni chachu katika kufanya kazi kwa ufanisi ikiwemo kufika maeneo mbalimbali kupitia doria, ukamataji na utoaji wa elimu ya Polisi Jamii kwa wananchi.
Jeshi la Polisi nchini kupitia Mkuu wa Jeshi hilo IGP Camillus Wambura ameendelea kutatua changamoto za vitendea kazi hususani magari kwa kuhakikisha yanapatikana ili kurahisisha utendaji kazi za Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.