RPC Malya: Ukatili wa kijinsia umepungua mkoani Songwe
16 January 2024, 10:36
Na Mwandishi wetu Songwe
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe kamishna msaidizi ACP Theopista Malya amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vimepungua mkoani Songwe kutokana na elimu inayotolewa kuifikia jamii.
Kamanda Malya ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ibada ya Jumapili alipotoa elimu ya ukatili katika kanisa la Kisima cha Uponyaji mjini Tunduma Januari 14, 2024.
Kamanda Malya ameongeza kuwa dalili za kuonesha kupungua kwa vitendo hivyo inatokana na kupungua kwa kesi za vitendo vya ukatili katika Dawati la Ukatili pamoja na Jamii kutoa taarifa za ukatili unapotokea au kutaka kutokea jambo ambalo linaonyesha elimu imefika kwa jamii.
“Nasema hali ni nzuri kwa sababu matukio ya ukatili ikiwemo ya ulawiti yamepungua kwa kiasi kikubwa, lakini pia tunapokutana na watu hivi tunaacha namba za simu kwa wachungaji, tukio lolote likitokea kwenye mtaa wowote tunapata taarifa.
Lakini pia imeonekana elimu hii ni muhimu kwa sababu tumekuwa na mialiko mingi ya kwenda kukutana na waamini kwa ajili ya kwenda kutoa elimu na kuwapa ufahamu namna ya kupambana na wahalifu na uhalifu.
Kama nilivyosema matukio haya yamepungua kwa sababu unaweza ukakaa kwenye dawati la jinsia wiki nzima usione mtu amekuja kuripoti na unaweza kukaa mwezi mzima ukapata tukio moja kwahiyo watu wameshajitambua wameelewa ukifanyiwa kitu gani ni ukatili kwahiyo wanatoa taarifa ambazo zinapelekea tunachukua hatua na matukio yanaendelea kupotea.
Aidha ameiasa jamii kuendelea kuchukua hatua kutokomeza matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ya ulawiti na ubakaji ambayo bado yapo katika jamii.