Songwe Dc yafanya ziara ya uripoti wa Wanafunzi shuleni
11 January 2024, 12:11
Na mwandishi wetu, Songwe
Wakuu wa Divisheni ya Elimu Awali, Msingi na Sekondari wamefanya ziara ya kufuatilia hali ya uripoti wa wanafunzi wanaoanza elimu ya awali, darasa la kwanza na wanaojiunga na kidato cha kwanza katika baadhi ya shule zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.
Shule zilifunguliwa Januari 8, 2024 ambapo tangu siku hiyo wanafunzi wanaendelea kuripoti shuleni huku wakuu wa divisheni na maafisa elimu wakakiendelea na ziara ya ufuatiliaji wa mwenendo wa wanafunzi wanavyoripoti shuleni katika Wilaya ya Songwe.
Ziara hiyo inaongozwa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Awali na Msingi Wilaya ya Songwe, Mwalimu Bunka Mtogolo pamoja na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Wilaya ya Songwe, Philipo Malika lakini pia ziara hiyo iliambatana na Afisa Mipango wa Wilaya ya Songwe kwaajili ya kusikiliza kero mbalimbali.
Aidha, wakuu hao wamesema kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri ambapo wametoa maagizo kwa walimu wakuu kuwaruhusu wanafunzi kuripoti shuleni hata kama hawana sare za shule ili waendelee na masomo wakati wazazi wao wakiendelea kukamilisha taratibu za kuwapatia sare na mahitaji mengine.
Viongozi hao wametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wote waliofikisha umri wa kuanza elimu ya awali na msingi pamoja na waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaripoti shuleni na kuhimiza wazazi wasiwafiche watoto wenye mahitaji maalumu kwa sababu elimu ni haki ya kila mtoto.