SACP Misime: Toeni malezi bora kutengeneza kizazi bora cha kesho
2 January 2024, 18:21
Na mwandishi wetu
Waumini wa kanisa la EAGT Kati kwa Mchungaji Alfred Mahenge lililopo kata ya Mlowo wilayani Mbozi wametakiwa kuwapa malezi bora watoto wao ili kutengeneza kizazi bora kwa maendeleo ya taifa.
Hayo yalisemwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP David Misime wakati aliposhiriki ibada kanisani hapo na kutoa elimu kwa waumini walioshiriki ibada hiyo kuhusu umuhimu wa malezi bora kwa watoto na kuwajenga kiimani ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu sambamba na vitendo vya mmomonyoko wa maadili.
Msemaji wa Jeshi la Polisi SACP Misime alisema kuwa, malezi bora kwa watoto wetu yanaanza na maelewano katika ndoa kama mnaishi vizuri bila migogoro kwenye ndoa zenu bila shaka watoto wenu watajifunza tabia njema na watakuwa wazazi wazuri wa watoto wao katika maisha yao ya baadae na tutapata kizazi bora ambacho kinafata mila na desturi za Mtanzania.
SACP Misime aliongeza kuwa kumcha Mungu ni kuyatenda yale yote aliyoyaelekeza katika biblia na vitabu vitakatifu pia kuyaishi ikiwa ni pamoja na kuwabariki watoto wetu toka wakiwa wadogo kwa yale mema wayafanyayo ili kutokomeza vitendo viovu katika jamii na hapo tutakuwa tumetengeneza kizazi bora na familia isiyokuwa na mhalifu.
“Nawaomba wazee mliopo kweye ibada hii mkae na wajuuku zenu kama mlivyokuwa mnakaa na sisi kwa lengo la kuwaadithia hadithi za kwenye Biblia na kuwafundisha malezi bora kwa watoto kama kwa lengo la kumjenga mtoto kwenye malezi mema ambayo yatapelekea kuwa na kizazi bora kwa mustakabari wa nchi yetu”. Alisema SACP Misime.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya ambaye naye alishiriki ibada hiyo alisema kasi ya utoaji elimu kwa jamii imeongezeka na wananchi wamekuwa wakitoa taarifa za matukio mbalimbali jambo ambalo limesababisha kupungua kwa uhalifu na wahalifu mkoani Songwe.
Nae mchungaji wa kanisa hilo Alfred Mahenge amelishukuru kwa dhati Jeshi la Polisi kwa elimu waliyoitoa na ameahidi kuendelea kukemea vitendo viovu kupitia waumini wake ili kupunguza matendo maaovu katika jamii.