Madereva wa mabasi ya abiria watakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani
21 December 2023, 09:56
Na Hobokela Lwinga
Kuelekea mwisho wa mwaka, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya Kikosi cha Usalama barabarani limewataka madereva wa Mabasi ya Abiria yanayofanya safari mikoa mbalimbali kuzingatia, kufuata na kuheshimu sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali na kuhakikisha abiria wana safari na kufika salama.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu wa Polisi Hussein Gawile wakati akifanya ukaguzi wa Mabasi ya Abiria Stendi Kuu ya Mabasi Mbeya kabla ya Mabasi hayo hayajaanza safari.
Mrakibu wa Polisi Gawile amesema kuwa, katika ukaguzi uliofanywa na wakaguzi wa magari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama barabarani (Vehicle Inspectors) jumla ya mabasi ya abiria 45 yalikaguliwa kati ya hayo mabasi 5 yalikutwa na kasoro ndogo ndogo ambazo wahusika walizirekebisha na kuruhusiwa kuanza safari.
Aidha, Mwenyekiti wa Mabalozi wa usalama barabarani Mkoa wa Mbeya ndugu Furaha Malele amewataka abiria kupaza sauti kukemea vitendo vinavyohatarisha usalama wao wakiwa kwenye vyombo vya moto, “Abiria mnao wajibu wa kupaza sauti dhidi ya vitendo vinavyofanywa na madereva ambavyo vinaweza kusababisha ajali na sio kufumbia macho” alisema Furaha Malele.
Naye, Abiria aliyekuwa akisafiri kutokea Mbeya kuelekea Songea ndugu Emanuel Kapinga amelipongeza Jeshi la Polisi kwa elimu na ukaguzi unaoendelea kufanyika wa Mabasi ya Abiria na kusema wao kama abiria wanachotaka na kusafiri salama na kufika salama na kuwataka madereva kuepuka mwendo kasi.
Dereva wa Kampuni ya usafirishaji ya “Premier Express” ndugu Abdallah Mtavava ametoa rai kwa madereva wenzake kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuwa na udereva wa kujihami ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Kuelekea mwisho wa mwaka, Jeshi la Polisi nchini kupitia kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na wadau wa usafirishaji LATRA, RSA na wengine, limejipanga vizuri kuhakikisha madereva wanakumbushwa wajibu wao ikiwemo kuzingatia sheria za usalama barabarani, abiria wanapewa elimu na kutambua wajibu wao wakiwa safarini ili kuepuka ajali na madhara mengine.