Mkuu wa mkoa wa Songwe akabidhi msaada kwa wafungwa gereza la vwawa
9 December 2023, 08:00
Na mwandishi wetu,Songwe
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Dkt Francis K. Michael kwa kushirikiana na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Songwe amekabidhi Tarehe 07 Desemba,2023 msaada wenye thamani ya zaidi shilingi milioni 3 kwa wafungwa wa Gereza la Vwawa wilayani Mbozi ikiwa ni kilele cha kuhitimisha wiki ya mlipa kodi nchini.
Akizungumza wakati wa kujabidhi msaada huo, Dkt. Francis Michael amesema kuwa jamii inatakiwa kutambua kuwa wafungwa nao ni raia na kufungwa ni sehemu ya mafunzo si laana kama inavyotafsiriwa huku akiishukuru TRA kwa kuwathamini wafungwa kwa msaada huo.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Songwe aneitaka jamii kuunga mkono jitihada za kuwasaidia wafungwa hao.
Aidha Dr. Michael amesema kuwa katika kushughulikia changamoto za magereza tayari gereza kubwa limejengwa wilayani Songwe ili litakapokamilika litapunguza msongamano katika gereza hilo la Mbozi,huku akiwataka wananchi kutambua umuhimu wa ulipaji kodi kwani kodi ndio huchangia kukuza uchumi na kuboresha huduma za kijamii nchini.
Kwa upande wakw Meneja wa TRA mkoani Songwe, Dickson Qamara amesema kuwa wamekabidhi
magodoro 50, mablanketi 50, dawa za meno, miswaki na mafuta pamoja na saruji mifuko kumi itakayotumika kujenga kituo cha afya ndani ya gereza hilo ikiwa ni sehemu ya krejesha kwenye jamii.