Pimeni afya zenu ili muishi vizuri
2 December 2023, 07:17
Na Hobokela Lwinga
Jamii mkoani mbeya imeombwa kujitokeza kwenye hospitali vituo vya afya, na zahanati kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza virusi mara moja hasa mhusika agundulikapo kuwa na maambukizi ili kuendelea kuijenga afya yake na kuishi maisha yenye furaha kama wanadamu wengine.
Hayo yamejiri leo katika sherehe za maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani ambapo kwa mkoa wa mbeya yamefanyika wilayani rungwe na kuhudhuliwa na wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na mkuu wa wilaya ya rungwe mh:jaffary haniu ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa comrade juma zuberi homera.
“naomba nitoe wito kwa wananchi wote mkoani mbeya kujitokeza kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi na ni vema ukaanza kutumia dawa za kufubaza virusi mara moja ili uendelee kuishi vizuri na ndugu jamaa na marafiki”. Amesema haniu ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Haniu katika hotuba yake mbali na kutoa wito kwa wananchi mkoani mbeya kujitokeza kupima maambukizi lakini pia amewataka wahudumu wa afya wanaotekeleza afua za ukimwi kubuni mbinu ya utoaji elimu kwa jamii juu ya upimaji afya kwa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii makanisa na wasanii wazawa.
Maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani hufanyika kila mwaka decemba 1 na mkoa wa mbeya umekuwa ni mshiriki mzuri wa maadhimisho hayo ambapo mbali na huduma ya upimaji kwa washiriki wa maadhimisho lakini pia hutolewa huduma ya uchangiaji damu kwa kila mshiriki aliye tayari.