Momba kusimamiwa na serikali ujenzi wa vyoo kwa gharama zao
8 November 2023, 15:35
Serikali ya halmashauri ya wilaya ya Momba imewaagiza watendaji wa vijiji na kata kutumia sheria ndogo za maeneo yao kutoza faini kwa wananchi ambao hawana vyoo bora na kuzitumia katika ujenzi wa vyoo bora kwa kaya ambazo zimetozwa faini hiyo kwa usimamizi mkali wa serikali hadi choo kikamilike.
Na mwandishi wetu,Momba Songwe
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Momba, Mhe. Methew Chikoti amesema hayo akiwa katika ziara maalum ya ukaguzi wa vyoo bora kwa ngazi ya kaya kwa kaya pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kwenye mikutano.
Mhe. Methew Chikoti amesema fedha itakayotozwa kwa mwananchi kutokana na ukosefu au kutokamilika kwa choo bora itakwenda kuboresha choo chake kutokana na mapungufu yake kwa faini atakayotozwa na serikali ya kijiji.
Pia, Mhe. Chikoti amewasisitiza wananchi ambao hawana choo bora kuuza baadhi ya mazao yao au mifugo ili kuweza kukamilisha ujenzi wa choo bora kwa kuwa nyumba ni choo bora.
Wakati huohuo, Mhe. Chikoti amewataka wananchi kuzingatia usafi wa mazingira kwenye kaya zao pamoja na maeneo ya biashara.